TANESCO YABAINI MATUKIO YA WIZI WA UMEME KINONDONI KASKAZINI



Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limebaini matukio ya wizi wa umeme katika eneo la Visiwani, Mwananyamala na Mivumoni, zilizo Wilaya ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam, wakati wa operesheni ya ukaguzi wa mita na miundombinu ya umeme inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.


Operesheni hiyo inalenga kudhibiti matumizi yasiyo halali ya umeme, kulinda miundombinu ya Shirika na kuhakikisha huduma ya umeme inaendelea kutolewa kwa usalama na ufanisi kwa wananchi.


Akizungumza wakati wa operesheni hiyo, Afisa Usalama wa TANESCO, Lilian Nizim, amewataka wananchi kuzingatia sheria na taratibu za matumizi ya umeme na kuepuka vitendo vya kuingilia au kuchezea mita za umeme.


Kwa upande wake, Mhandisi wa TANESCO Mkoa wa Kinondoni Kaskazini, Mha. Underson Manyika, amesema wakati wa ukaguzi katika eneo la Visiwani, timu ya wataalamu ilibaini baadhi ya wateja wakiwa wamechepusha nyaya za umeme, hali iliyosababisha mita kutosoma matumizi halisi ya umeme.


Amesema vitendo vya wizi wa umeme husababisha hasara kwa Shirika, kuhatarisha usalama wa wananchi na kuathiri ubora wa huduma ya umeme, hivyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na TANESCO kwa kutoa taarifa za vitendo hivyo ili viweze kudhibitiwa kwa wakati.







No comments