ULEGA: PWANI KITUO CHA VIFAA VYA DHARURA, AAGIZA TANROADS, TARURA KUKAGUA MADARAJA, MITARO
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Mkoa wa Pwani umewekwa kuwa kituo kikuu cha kuhifadhi vifaa vya dharura vitakavyotumika kukabiliana na athari za mvua za El Nino, huku vituo vingine vikiwa katika Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kusini.
Ulega amesema hayo alipowasili mkoani Pwani kwa ajili ya kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujiandaa mapema kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Amesema vifaa vilivyohifadhiwa Pwani vikiwemo makaravati ya chuma, vikapu vya mawe na madaraja ya chuma vinapaswa kuwa tayari kutumika wakati wowote, huku akisisitiza ukaguzi na usafishaji wa mitaro, makaravati na madaraja ili kuhakikisha maji yanapita kwa uhuru na kuzuia barabara kukatika.
Ulega pia ameiagiza TANROADS na TARURA kufanya tathmini za mara kwa mara katika maeneo hatarishi, akisisitiza tathmini hizo kufanyika kila wiki ili kuongeza nguvu katika maeneo ambayo yanaweza kuzidiwa na mvua na kuhakikisha hakuna barabara inayofungwa.
Katika hatua nyingine, amemtaka Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani kusimamia wakandarasi ambao hawajalipwa, huku akiwataka wakandarasi kuendelea na utekelezaji wa majukumu yao na kutoa ushirikiano katika kipindi hiki cha maandalizi.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Pwani, Mhandisi Joel Mwambungu, amesema wamejipanga katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kusafisha madaraja, mitaro na makaravati, huku akitaja eneo la Ruvu Chini kuwa miongoni mwa maeneo yanayofanyiwa kazi kwa kusafisha kingo za mto ili kuruhusu maji kupita kwa kiwango kilichosanifiwa.










Post a Comment