BALOZI MINDI AFUNGUA KONGAMANO KUMUEZI DKT SALIM NA KUTOA WITO HUU KWA VIJANA

Picha na, Wizara ya Mambo ya Nje.

Septemba 30, 2026 katika Kituo Cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, kulifanyika Kongamano la Pili la kumuenzi Dkt. Salim Ahmed Salim, ambalo lilifunguliwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mindi Kasika. 


Kufanyika kwa kongamano hilo kunalenga kutafakari urithi wa Dkt. Salim na umuhimu wa mchango wake katika historia ya Diplomasia ya Afrika na Dunia.


Akifungua Kongamano hilo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi alisema Tanzania inatambua mchango mkubwa wa Dkt. Salim katika diplomasia ya Tanzania na kimataifa, hususani katika kuendeleza amani, kusuluhisha migogoro, kuimarisha mshikamano wa Afrika, na kutetea nafasi na maslahi ya nchi zinazoendelea katika Mfumo wa Kimataifa.


Amesema Dkt. Salim, ni miongoni mwa Watanzania waliotoa mchango mkubwa katika kuiwakilisha Tanzania na Afrika katika majukwaa ya kimataifa, kupitia utumishi wake katika balozi mbalimbali duniani, zikiwemo Misri, India na China, pamoja na Umoja wa Mataifa.


Balozi Mindi amebainisha kuwa urithi wa Dkt. Salim haupaswi kupimwa kwa kuangalia idadi ya nyadhifa alizowahi kushika pekee, bali pia kwa kuzingatia maadili yake katika utumishi, hekima, busara na mtazamo wake kuhusu nafasi ya Tanzania na Afrika katika ulimwengu.


Amewataka Vijana Vijana kuenzi urithi wa Dkt. Salim kwa kutumia diplomasia katika kukuza mazungumzo ya amani na kutatua migogoro ndani na nje ya nchi, hatua itakayochangia kujenga uaminifu na kuwezesha suluhisho endelevu la migogoro.


“Urithi wa Dkt. Salim unatukumbusha nguvu ya maarifa, nidhamu, uadilifu, uvumilivu, kusikiliza na kujenga mahusiano katika diplomasia. Tumieni teknolojia mpya, ikiwemo Akili Unde (AI), kuendeleza maslahi ya Tanzania na Afrika, huku wakilinda misingi ya utu, maadili na uwajibikaji,” alisema Balozi Mindi.

Kufanyika kwa Kongamao hili, ni muendelezo wa Serikali ya Tanzania kutambua na kuthamini kazi kubwa iliyofanywa na viongozi mbalimbali walioongoza katika nafasi za juu serikalini ili kuonesha mshikamano na umoja wa kitaifa, huku vijana wakilengwa zaidi katika kuwafanya watambue kazi kubwa iliyofanywa na viongozi hao.


No comments