MICHE ZAIDI YA ELFU HAMSINI YA MITI KUTAYARISHWA GEREZA MGAGAO
Na. Gishing'ida Masauna – IRINGA
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Abdallah Missanga, Septemba 29, 2026, amekagua vitalu vya miche ya miti zaidi ya 50,000 vinavyoandaliwa kwa ajili ya kupandwa Gereza Mgagao.
ACP Missanga, amepongeza uongozi wa Gereza hilo kwa maandalizi ya vitalu hivyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuwapatia wafungwa wanaoshiriki katika shughuli hizo elimu na ujuzi unaoweza kuwasaidia baada ya kumaliza vifungo vyao.
Aidha, ACP Missanga amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kituo hicho, ikiwemo bustani na shamba la parachichi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji na kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya kituo.
Katika ziara hiyo, pia amefanya baraza na wafungwa pamoja na askari, ambapo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano, nidhamu na kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya kituo, hususan katika uzalishaji na urekebishaji wa wafungwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza Mgagao, SP Msafiri Hamis Namkaa, amesema kituo hicho kinaendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za uzalishaji kwa lengo la kuhakikisha kinapata chakula cha kutosha pamoja na kuchangia katika ulipaji wa maduhuli ya Serikali.


Post a Comment