Tanzania inatarajia kupata dola za Marekani milioni 41.06 kupitia awamu ya tisa ya Mfuko wa Dunia wa Mazingira
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dkt. Maduhu Isaac Kazi, amesema Tanzania inatarajia kupata dola za Marekani milioni 41.06 kupitia awamu ya tisa ya Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF-9), zitakazosaidia kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Kazi alisema hayo wakati wa ufunguzi wa mazungumzo ya kitaifa ya GEF-9 yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, akieleza kuwa Tanzania imenufaika na takribani dola milioni 53.4 kupitia awamu ya nane ya mfuko huo. Alisema ufadhili huo ni fursa ya kuendeleza juhudi za uhifadhi wa misitu, bioanuai, udhibiti wa uchafuzi na urejeshaji wa ardhi iliyoharibika.
Alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na washirika wa maendeleo ili kuweka vipaumbele vya pamoja na kuhakikisha uwekezaji wa mazingira unachangia maendeleo endelevu ya taifa.
Akizungumza katika mkutano huo, Mtaalamu Mwandamizi wa Mazingira na Mratibu wa Kanda ya Afrika wa Sekretarieti ya GEF, Jonky Tenou, alisema mazungumzo hayo yanatoa fursa kwa Tanzania kutathmini mafanikio ya miradi iliyopita, kubaini mapungufu na kuandaa vipaumbele vya uwekezaji kwa awamu mpya.
Tenou alisema GEF-9 inalenga kuimarisha uratibu wa sera, kuchochea ubunifu na kuongeza ushirikiano katika miradi inayohusu bioanuai, mabadiliko ya tabianchi, uharibifu wa ardhi, kemikali na taka pamoja na rasilimali za maji ya kimataifa. Alisema ushiriki wa Serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na washirika wa maendeleo ni muhimu katika kuandaa miradi yenye manufaa ya kimazingira, kijamii na kiuchumi.
Aliongeza kuwa matokeo ya mazungumzo ya hivi karibuni kuhusu ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi nchini yanaweza kusaidia kuboresha vipaumbele vya uwekezaji wa mazingira na kuongoza maandalizi ya miradi ya GEF-9.
Kwa upande wake, SACC Fandey H. Mashimba, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Meneja wa Sehemu ya Baiolojia ya Mbegu za Miti kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Profesa Dos Santos Silayo, alisema wakala huo unatafuta fursa zaidi za ufadhili zitakazosaidia kuimarisha uhifadhi wa misitu na rasilimali za nyuki pamoja na kuendeleza utalii katika hifadhi zake.
Mazungumzo hayo ya siku mbili, yanafanyika kuanzia Leo, Oktoba 12–13, 2026, katika Hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam, yakilenga kupitia matokeo ya miradi iliyopita, kubainisha vipaumbele vya kitaifa na kuandaa mapendekezo ya miradi yatakayoweza kupata ufadhili kupitia GEF-9.

Post a Comment