Jeshi la Magereza laepuka kuzalisha madeni ya wazabuni chakula cha Wafungwa
Mkuu wa Jeshi la Magereza, CGP. Jeremiah Yoram Katungu amesema Jeshi la Magereza limefanikiwa kuepuka kuzalisha madeni mapya kwa wazabuni wa chakula cha wafungwa kuanzia Julai hadi Novemba 2026, hatua inayotokana na kuimarika kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo ndani ya Jeshi la Magereza.
CGP Katungu, amesema mkakati huo unalenga kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama za uendeshaji huku ukihakikisha wafungwa na mahabusu wanapata lishe bora kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza jijini Arusha wakati akifungua kikao cha Baraza Dogo la Wafanyakazi wa Jeshi la Magereza (TUGHE), Kamishna Jenerali Katungu, alieleza kuwa lengo kuu ni kumaliza mwaka mzima wa fedha wa 2026/2027 bila deni lolote la huduma ya chakula.
Katika kikao hicho kilichojadili utekelezaji wa robo ya kwanza ya bajeti, Mkuu Jeshi la Magereza pia alibainisha maboresho makubwa ya kiutawala na rasilimali watu yaliyofanyika hivi karibuni kupitia Serikali ya awamu ya sita kwa kuajiri askari wapya 1,561 ili kuongeza nguvu kazi, kuwapandisha vyeo maafisa na askari 773, wakiwemo Manaibu Kamishna 17 na Makamishna Wasaidizi Waandamizi 22 idadi hiyo kuwa kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa kwa wakati mmoja ndani ya Jeshi la Magereza. Pamoja na kuwapandisha vyeo watumishi raia 16 na wengine watatu kupandishwa madaraja.
Hata hivyo, CGP Katungu alitoa tahadhari kwa viongozi wa chama cha wafanyakazi (TUGHE), akiwataka kutotumia jukwaa hilo kuchochea migogoro au kutetea uzembe na uvivu kazini.
"Chama kiwe chachu ya kuhimiza uwajibikaji na kusimamia upatikanaji wa haki kwa pande zote mbili ya mwajiri na wafanyakazi kwa kuwa hakuna haki bila kutekeleza wajibu," alisisitiza CGP Katungu.
Kwa upande wake, Kamishna wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, CP Ahmad Mwen- Dadi, amesema uwepo wa Baraza hilo umeongeza ari ya uchapakazi na uwazi katika utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Jeshi.
Ameongeza kuwa pamoja na majukumu ya ulinzi na urekebishaji wa tabia za wafungwa, Jeshi la Magereza linaendelea kuzingatia misingi ya utu, haki za binadamu, na mikataba ya kimataifa katika shughuli zake za kila siku.
Kwa mtazamo wa Onemedia, hatua ya Jeshi la Magereza kutozalisha madeni ya wazabuni, kunaipunguzia Serikali mzigo wa kuhudumia Wafungwa, na endapo jitihada hizi zitakuwa endelevu, Jeshi la Magereza litapiga hatua kubwa katika kuiletea Nchi maendeleo.

Post a Comment