TANZANIA YAHIMIZA USHIRIKIANO WA KIKANDA KUONGEZA THAMANI MADINI BARANI AFRIKA
Akitoa mchango katika mdahalo wa Mawaziri wa Madini wa Kongo DRC, Zambia, Burundi na Chad, Waziri wa Madini *Mhe. Anthony Mavunde (Mb)* abainisha na kuhimiza umuhimu wa ushirikiano wa Kikanda katika kuongeza thamani madini Barani Afrika.
Ameyasema hayo leo tarehe 24 Novemba, 2026 alipomwakilisha Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Madini ujulikanao kama Makutano 2026 uliofanyika Jijini Kinshasa nchini Kongo DRC.
"Tanzania ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Madini ambayo yalipelekea kuzuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya Nchi, imeweka ulazima wa kuongezwa thamani ndani ya Nchi kabla ya kuuzwa nje"
"Kufuatia marufuku hiyo, tumeanza kuona hamasa ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini ambapo kwa upande wa dhahabu kuna zaidi ya viwanda 8 vya kusafisha dhahabu. Vilevile, kwa upande wa madini ya metali (base metals) kama shaba na nikeli tumeona zaidi ya viwanda 16 vimejengwa nchini kwetu" alisisitiza Waziri Mavunde.
Pamoja na hilo, Waziri Mavunde alieleza umuhimu wa kongani ya viwanda ya Buzwagi iliyopo Kahama Mkoani Shinyanga, ambapo panatarajiwa kujengwa Kiwanda chenye teknolojia ya kisasa ya kuongeza thamani madini ya shaba na nikeli.
"Kupitia kiwanda cha kimkakati kitakachojengwa Kahama, tunatarajia si tu kiongeze thamani madini kutoka Tanzania, bali kutoka Nchi jirani zikiwemo Burundi na Kongo. Hili limewekewa mkazo madhubuti kupitia ujenzi wa reli ya kisasa ya Isaka mpaka Musongati Burundi, pamoja na ujenzi wa bandari za Karema na Karemii ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma" aliongeza Waziri Mavunde.
Awali, akifungua rasmi mkutano huo wa madini wa Makutano 2026, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mhe. Felix Tshisekedi
Tshilombo ameweka bayana msimamo wa Nchi ya Kongo kwamba suala la kuongeza thamani si hiari tena, ni lazima mwekezaji au mtu yeyote atakayechimba madini Kongo ayaongeze thamani kabla ya kuyasafirisha Nje.
Aidha, Mhe. Tshisekedi amebainisha kwamba, suala la msingi linatakiwa lisiwe ni kiasi gani cha madini ya shaba, cobalt au lithium Kongo imezalisha, bali iwe ni manufaa gani ya kiuchumi yamepatikana ndani ya Nchi kutokana na uchakataji, usafishaji, utengenezaji, uhaulishaji wa teknolojia na maendeleo ya viwanda kupitia madini hayo yaliyozalishwa.


.jpeg)
.jpeg)



.jpeg)


Post a Comment