TANESCO yatekeleza maagizo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi



Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limetekeleza maagizo ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, kwa kufunga transfoma mpya na kubwa yenye uwezo wa MVA 150 katika kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Ibadakuli mkoani Shinyanga, hatua inayolenga kumaliza kabisa changamoto ya upungufu wa umeme mkoani Katavi.

Hatua hiyo ni matokeo ya ziara ya kikazi ya Makamu wa Rais aliyoifanya ambapo akiwa katika Uwanja wa Ndege wa Mpanda, alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Lazaro Twange, kuhakikisha TANESCO inaboresha hali ya upatikanaji wa umeme mkoani Katavi ifikapo tarehe 01 Desemba, 2026 ambapo TANESCO imekamilisha Jumapili ya Novemba 15, 2026.

Akiongelea hali ya upatikanaji wa umeme mkoani Katavi baada ya marekebisho Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Katavi, Mhe. Idd Kimanta amesema Mkurugenzi Mtendaji TANESCO,  Lazaro Twange aliahidi mbele ya Makamu wa Rais hadi kufikia Disemba moja Mkoa wa Katavi utakuwa na umeme wa uhakika.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Katavi, Mha. Florence Mwakasege amesema upatikanaji wa umeme Mkoa wa Katavi kwa hivi sasa umeimarika na kutoa rai kwa wananchi kuendelea kufanya maombi ya kuunganishiwa umeme kwani upo wa kutosha.

Akiongea kwa niaba ya Wafanyabiashara Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Katavi, Aman Mahela ameipongeza TANESCO kwa kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais kabla ya wakati ambao walikuwa wamepangiwa na kuhakikisha Mkoa wa Katavi unakuwa na umeme wa uhakika.









No comments