TANZANIA INAHITAJI KUJIANDAA NA ONGEZEKO LA WATU MILIONI 123 IFIKAPO 2044
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), David Kafulila, amesisitiza umuhimu wa Tanzania kuwekeza zaidi katika rasilimali watu ili kukabiliana na ongezeko kubwa la idadi ya watu nchini, akieleza kuwa ongezeko hilo linaweza kuwa fursa ya kukuza uchumi au changamoto endapo halitaandaliwa ipasavyo.
Akizungumza jijini Dar es salaam katika kikao cha kupima mwitikio wa sekta binafsi kuhusu miradi ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Kafulila, amesema idadi ya Watanzania imeongezeka kutoka milioni 44.9 mwaka 2012 hadi zaidi ya milioni 61 mwaka 2022, huku makadirio yakionyesha kuwa idadi hiyo itafikia milioni 123.4 ifikapo mwaka 2044.
Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 42.8 ya Watanzania wana umri chini ya miaka 15, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuwekeza mapema katika elimu, afya, maarifa na ujuzi ili kuwaandaa vijana hao kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na uzalishaji.
Hata hivyo, amesema uwekezaji wa sasa katika sekta hizo bado ni mdogo, ambapo Tanzania inatumia asilimia 3.3 ya Pato la Taifa (GDP) katika elimu na asilimia 1.2 katika sekta ya afya, viwango ambavyo amesema viko chini ya wastani wa nchi zenye kipato cha chini cha kati.
Kutokana na hali hiyo, Kafulila, ameeleza kuwa matumizi ya mfumo wa PPP ni miongoni mwa njia zinazoweza kusaidia Serikali kushirikiana na sekta binafsi katika kujenga na kuendesha miundombinu ya kibiashara, ikiwemo masoko, majengo na maegesho.
Ushirikiano huo amesema utasaidia kupunguza mzigo wa uwekezaji wa Serikali katika miundombinu ya kibiashara na kuwezesha rasilimali zaidi kuelekezwa katika huduma muhimu za kijamii, hususan elimu na afya, ili kuhakikisha ongezeko la idadi ya watu linakuwa chachu ya maendeleo badala ya kuwa mzigo kwa Taifa.


.jpeg)

Post a Comment