TANZANIA YAPONGEZWA MATUMIZI YA VIWANGO VYA KIMATAIFA VYA UHASIBU WA SEKTA YA UMMA
Tanzania imepongezwa kwa kuwa miongoni mwa nchi kinara barani Afrika kutumia viwango vya kimataifa vya Uhasibu wa Sekta ya Umma (IPSAS), hatua iliyochangia kuweka uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma.
Pongezi hizo zimetolewa mjini Accra, Ghana na Mshauri wa masuala ya matumizi ya viwango vya kimataifa vya uhasibu kutoka Zimbabwe, Bw. Amon Dhlimayo, wakati akitoa mada kuhusu matumizi ya viwango hivyo wakati Mkutano wa Tatu wa Wahasibu wa Serikali Barani Afrika (African Association of Accountants General Meeting (AAAG), unaofanyika nchini humo.
Alisema kuwa Tanzania ilikuwa nchi ya mwanzo kabisa katika Bara la Afrika kutumia viwango hivyo vya kimataifa vya uhasibu, hatua iliyochangia nchi kuwa na taarifa za fedha zenye viwango na zinazokubalika kimataifa.
Aliziasa nchi nyingine kufuata nyayo za Tanzania na baadhi ya nchi nyingine za Afrika, kutumia mfumo huo wa usimamizi wa fedha za umma unachangia taarifa za fedha kuwafikia wananchi na hivyo kuchangia maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake, Mhasibu Mkuu wa Serikali ya Tanzania, CPA Leonard Mkude, alisema kuwa matumizi ya viwango vya kimataifa wa uhasibu wa fedha za Umma (IPSAS), umekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa usimamizi na udhibiti wa fedha za umma umekuwa wa kiwango kikubwa, zinawekwa wazi na kujadiliwa na makundi mbalimbali ikiwemo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vinachochea msukumo wa kisera na kutumia Uhasibu wa Ujumuishaji kwa Uboreshaji wa Usimamizi wa Mali na Madeni.
Mkutano huo uliobeba Kaulimbiu isemayo “Afrika ya Kesho: Kuimarisha Usimamizi wa Fedha za Umma kwa ajili ya Ustawi wa Kiuchumi", umewahusisha washiriki zaidi ya 2,000 kutoka nchi 55 za Afrika, umelenga kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kusimamia matumizi sahihi ya fedha za umma.


.jpeg)
Post a Comment