TANAPA YASHINDA TUZO YA UBORA YA KIMATAIFA KWA MWAKA 2025 – ESQR

 

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) leo Desemba 09,2025 limepokea Tuzo ya Utoaji Huduma Bora ya Kimataifa  kwa mwaka 2025 (Quality Achievements Awards 2025), tuzo zinazotolewa na taasisi ya European Society for Quality Research (ESQR) iliyoko Lausanne, Uswisi. Huu ni ushindi wa mara ya 7 mfululizo tangu mwaka 2020, ikitambua ubora  wa TANAPA katika sekta ya uhifadhi na utalii Tuzo hiyo ilitolewa katika hafla ya Tuzo zilizofanyika hoteli ya  Dusit Thani Dubai - Umoja wa Falme za Kiarabu.


Kwa mwaka huu, taasisi 49 kutoka jumla ya nchi 41  duniani zimenyakua tuzo hizi ikiwemo  Shirika  la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kutoka Sekta ya Uhifadhi na Utalii lakini pia taasisi nyingine zilizotambuliwa katika utoaji Huduma bora ni pamoja na sekta za Afya, Elimu, Ujenzi, Jamii, Uhifadhi , Utalii, Madini, Teknolojia na sekta nyinginezo.


Misingi ya Maadili ya TANAPA, ambayo ni Utaalamu, Uwajibikaji, Uadilifu, Ushirikiano, Ufanisi, Ubunifu, na Ubora, pamoja na kanuni za usimamizi wa ubora za Shirika la Kiwango cha Kimataifa (ISO), zimeendelea kuwa mwongozo muhimu katika dhamira yake ya kutoa huduma bora za uhifadhi na utalii. Misingi hii inahakikisha kwamba huduma zinazotolewa na TANAPA zinakidhi viwango vya kimataifa, na hivyo kuimarisha nafasi yake katika sekta ya uhifadhi na utalii duniani.


Ushindi wa TANAPA katika tuzo hii, si tu fahari ya shirika, bali pia ni ushindi mkubwa kwa nchi yetu ya Tanzania. Ni ishara ya kujitolea kwa taifa letu katika kuhifadhi na kutangaza urithi wetu wa asili, huku tukionyesha dunia umuhimu wa maliasili zetu na uhifadhi wa mazingira. TANAPA, kupitia huduma bora na juhudi za dhati, imeweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa kama kiongozi katika uhifadhi wa wanyamapori na utalii endelevu.


Hafla ya kupokea tuzo hiyo imeongozwa na  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Utalii Nkoba Mabula ambaye aliambatana  na CPA(T) Hadija Ramadhani Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, pamoja na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA CPA Musa Nassoro.

No comments