TANZANIA NI MFANO WA KUIGWA KWA AMANI DUNIANI - GUTTERES
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Antonio Guterres, amesema kuwa “Tanzania imekuwa ni rejea muhimu ya amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani kote,”
GUTTERES, amesema hayo leo, Desemba 14, 2025 wakati akipokea ujumbe maalum kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza kuwa taswira ya Tanzania ni kielelezo cha amani ambayo ilijaribiwa katika uchaguzi wa hivi karibuni uliofanyika Oktoba 29, 2025, lakini taifa liliweza kuvuka mtihani huo kwa mafanikio, ikiwa ni mara ya kwanza kukabiliwa na changamoto hiyo.
“Umoja wa Mataifa ungependa kuona Tanzania inaendelea kubaki katika umoja wake na kuwa mfano bora kwa mataifa mengine,” alisema Katibu Mkuu Guterres alipokuwa akipokea Ujumbe Maalum uliobeba salamu na ujumbe kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, uliowasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Kombo, pamoja na ujumbe wake.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mazungumzo ya kitaifa yenye maana, jumuishi na shirikishi ili kushughulikia chanzo cha matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29, pamoja na kutafuta njia za kudumu za kuyazuia yasijirudie tena.
Aidha, aliahidi msaada kamili wa Umoja wa Mataifa wakati wote na hata baada ya Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa nchini Tanzania kukamilisha majukumu yake.

Post a Comment