WATANZANIA WAHIMIZWA KUDAI HAKI WAKIADHIMISHA XMAS

Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa’ichi, amesema Watanzania wengi hawashabikii haki na si wadau wa haki, hali inayochangiwa na ujinga, kurubuniwa au kujidai kuwa wadau wa amani bila kuzingatia misingi ya haki.


Askofu Ruwa’ichi aliyasema hayo wakati wa ibada maalum ya mkesha wa kuadhimisha sikukuu ya Krismasi, ambapo aliwahimiza Wakristo wanaoadhimisha kuzaliwa kwa Mwokozi Yesu Kristo kuwa wadau wa haki katika maisha yao ya kila siku.


Akifafanua, Askofu Ruwa’ichi alisema Yosefu aliyemkaribisha Yesu nyumbani kwake anatambulika kama mtu wa haki, kwani aliweza kumlinda, kumtunza na kumkaribisha Maria kumlinda na kumtunza.


"Yosefu aliyemkaribisha Yesu nyumbani kwake anatambulika kama mtu wa haki, aliweza kumkaribisha Maria kumlinda na kumtunza, sisi sote kwa nguvu ya ubatizo wetu ambao umetufunganisha na Kristo Mwokozi tunaitwa tuwe watu wa haki...haki ni ule uelewa wa kutambua mastahili ya wengine na kuyaheshimu".


Alisisitiza kuwa Wakristo wote, kwa nguvu ya ubatizo wao unaowaunganisha na Kristo Mwokozi, wameitwa kuwa watu wa haki, akieleza kuwa haki ni uelewa wa kutambua mastahili ya wengine na kuyaheshimu ipasavyo.


Askofu huyo aliwakumbusha waumini kuwa haki ndiyo msingi wa amani ya kweli, akionya kuwa hakuna amani ya kudumu bila haki, hivyo kuwataka Watanzania kuwa wadau wa amani kwa kuanzia kwenye haki.


Katika mahubiri yake, aliuliza kwa msisitizo akisema, “Ewe mwana wa Dar es Salaam, ewe Mtanzania, je wewe ni mtu wa haki?” akilenga kuwahamasisha waumini kujitathmini binafsi.


Wakati huo huo, Wakristo kutoka Afrika Mashariki wameungana na wenzao duniani kote kuadhimisha sikukuu ya Krismasi, huku viongozi mbalimbali akiwemo Rais wa Kenya William Ruto na Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan wakitoa salaam za heri ya Krismasi kwa waumini.


Rais Samia Suluhu Hassan aliandika katika mtandao wa kijamii "Ninawatakia kheri ya sikukuu ya Krismasi wakristo wote na watanzania wote Mwenyezi Mungu awabariki nyote".


Naye rais Ruto alionekana katika video akiwatakia wakenya heri ya sikukuu na kuwaasa kuendesha vyombo vya moto kwa uangalifu kuepuka ajali.

No comments