BRELA YATOA ELIMU KWA WANAFUNZI WA SHULE YA SEKONDARI FEZA BOYS



Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa mafunzo kwa wanafunzi wanaosoma masomo ya biashara katika Shule ya Sekondari Feza Boys iliyopo Bahari Beach jijini Dar es Salaam.

Hatua hii inatokana na mabadiliko ya mtaala wa kufundishia ambao unawataka wanafunzi kusoma kwa nadharia na vitendo ikiwa ni pamoja na kupata elimu sahihi kutokana na uhalisia wake  kutoka taasisi husika.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo  Afisa Usajili kutoka BRELA,  Maryglory Mmary, alisema elimu hiyo inalenga kuwasaidia vijana kuelewa mapema taratibu za kisheria wakati wa kusajili biashara zao ili kuepuka changamoto wanapoingia katika shughuli za kibiashara baada ya masomo.

Aidha,  Mmary aliwaeleza kwa kina taratibu na vigezo vinavyohitajika katika kusajili majina ya biashara na kampuni huku akisisitiza umuhimu wa kufanya biashara kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo ili kupata ulinzi wa kisheria na fursa mbalimbali zinazotolewa na serikali.




Naye Afisa Sheria Calvin Rwambogo, alitoa elimu kuhusu Alama za Biashara na Huduma, akiwaeleza kuwa hizi hutumika kutofautisha bidhaa au huduma za mfanyabiashara mmoja na mwingine sokoni na zinaweza kuwa katika mfumo wa nembo, alama au chapa (logo).

Aidha, Calvin aligusia pia suala la ulinzi wa Hataza ambapo alisema ili uvumbuzi upewe hati ya hataza ni lazima uwe mpya na usiotambulika kwa umma, usiwe rahisi kwa mtu mwingine kuutumia, uwe na mchango wa kutatua changamoto katika jamii, na usiwe na ufanano na uvumbuzi uliosajiliwa tayari.

Mafunzo hayo ya urasimishaji wa biashara ni sehemu ya mkakati wa BRELA wa kuwajengea vijana uelewa wa masuala ya biashara na haki miliki wakiwa bado shuleni, ili kuandaa kizazi cha wafanyabiashara wanaofuata sheria, wenye ubunifu na wanaochangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi wa taifa.







No comments