RAS MANYARA AIPONGEZA MSD MATUMIZI YA MIFUMO YA KIDIGITALI.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Dominic Mbwette ameipongeza Bohari ya Dawa (MSD) kwa matumizi ya mifumo ya kidigitali kurahisha huduma na kuboresha utendaji.
Mbwette ametoa pongezi hizo hii leo, baada ya kutembelea banda la MSD kwenye maonesho maalum yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Serikali Mtandao, kando ya kikao cha sita cha Serikali Mtandao mwaka 2026.
Mbwette amesema maelezo aliyopokea yanaakisi jinsi MSD ilivyonipanga kuhakikisha huduma zake zinaendelea kuwa bora na kuongeza ufanisi.
Akitoa maelezo mbele ya kiongozi huyo, Afisa Tehama kutoka MSD John Nyanda, amebainisha jinsi MSD ilivyoweza kutengeneza mifumo mbalimbali kurahisisha utendaji kazi na kuboresha huduma, kama Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Uchumi 2050 inavyoainisha.
Nyanda ameanisha mifumo hiyo kwamba ni pamoja na mfumo wa WEMIS, unaotumika kufuatilia hali joto na jotoridi la bidhaa za afya ndani ya maghala, ambapo taarifa kutoka mifumo hiyo imewezeshwa kupitia simu za mkononi, na kupitia kompyuta.
Ameongeza kuwa mfumo mwingine unaotambulika kama "Fleet Management" unatumika kufuatilia mienendo ya magari na dereva, usambazaji bidhaa za afya, jotoridi na matumizi ya mafuta.
Vile vile, amebainisha uwepo wa mfumo wa MSD- Connect unaotumika kufuatilia na kusimamia mikataba, sambamba na mifumo mingine kama Customer Portal, na Epicor 10.
MSD ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki maonesho haya kwa mwaka 2026, yaliyopambwa na kaulimbiu isemayo " Huduma Bora za Umma Kupitia Teknolojia" ikilenga malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Uchumi 2050, ambapo zaidi ya asilimia 80 ya huduma za serikali zinatarajiwa kufanikishwa kidigitali.
Post a Comment