RC KHERI AWATAKA WAHANDISI WA UMWAGILIAJI KUTANGULIZA UZALENDO NA WELEDI KULINDA FEDHA ZA SERIKALI

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewataka Wahandisi wa Mikoa na Wasimamizi wa miradi ya Umwagiliaji nchini kufanya kazi kwa uzalendo wa hali ya juu na weledi ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali unaleta tija iliyokusudiwa kwa wananchi. 

Amesema hayo mkoani Iringa wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya kuwajengea uwezo watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) yaliyohusu Usimamizi wa Mikataba, Sheria za Ununuzi, Uhandisi wa Geoteknolojia (Utafiti wa Miamba) na ubadilishanaji wa uzoefu. 

Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa miongozo na fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha sekta ya Umwagiliaji , akibainisha kuwa miradi hiyo ni tegemeo kubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kukuza uchumi wa taifa. 
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa ameipongeza Tume ya Taifa ya Umwagiliaji chini ya Mkurugenzi Mkuu, Raymond Mndolwa, kwa kuimarisha weledi na kudhibiti migogoro inayokwamisha miradi. 

Amesisitiza kuwa bila msimamo wa kusimamia weledi, miradi mikubwa ikiwemo ile ya mabilioni ya fedha kama mradi wa Mkombozi ingebaki kuwa hadithi badala ya kuleta matokeo. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji  Mndolwa amesema Tume imejipanga kusimamia miradi ya umwagiliaji kwa karibu ili kuhakikisha inakamilika kwa ufanisi na kuleta tija kwa wakulima na taifa kwa ujumla. 
Mndolwa amesema NIRC inaendelea kujenga mabwawa ya Umwagiliaji, kuvuna na kuhifadhi maji pamoja na kutekeleza shughuli za uhifadhi wa mazingira, akieleza kuwa hatua hizo ni sehemu ya uzalendo wa kulinda rasilimali za Taifa ili kufikia adhima ya kuongeza uzalishaji wa mazao na kujitosheleza kwa chakula cha ndani na kuilisha Dunia.

No comments