SERIKALI YAIMARISHA USHIRIKIANO NA WADAU UHIFADHI WA MALIASILI NA KUKABILIANA NA WANYAMAPORI WAKALI
Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa uhifadhi katika kuimarisha ulinzi wa maeneo yaliyohifadhiwa sambamba na kukabiliana na changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu wanaovamia mashamba na makazi ya wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb.) jijini Dodoma alipokutana na kuzungunza na ujumbe wa Shirika lisilo la Kiserikali la Six Rivers Afrika kwa lengo la kuweka mikakati ya kuimarisha ulinzi katika maeneo ya hifadhi hapa nchini
"Tunawashukuru wote kwa kuendelea kushirikiana nasi katika uhifadhi, na maswala mbalimbali ya kifedha kuwezesha uendeshaji wa shughuli za uhifadhi na sekta ya utalii hivyo nasi kama Serikali milango yetu ipo wazi muda wowote katika kuimarisha na kuendeleza sekta ya uhifadhi hapa nchini" amesisitiza Mhe. Chande
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo Bw. Glenn Turner ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza ushirikiano uliopo na Shirika hilo huku akisisitiza kuendeleza mipango mbalimbali ya ufuatiliaji wa mienendo ya wanyamapori na bioanuwai katika Hifadhi za Taifa Nyerere na Ruaha kwa kutumia mfumo wa data zilizounganishwa kwa kutumia G.P.S Collars na ujenzi wa miundombinu.
Shirika la Six Rivers Afrika limekuwa likifadhili shughuli mbalimbali za uhifadhi kwa kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi kama magari na boti; ujenzi wa majengo ya vituo vya kiikolojia; ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano katika maeneo ya hifadhi; ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya viwanja vya ndege na kuanzisha miradi inayonufaisha jamii inayozunguka maenel yaliyohifadhiwa.
Post a Comment