TPDC YATAKIWA KUFANYIA KAZI MAELEKEZO YA VIONGOZI WAKUU KUKAMILISHA MIRADI YA KIMKAKATI

Watendaji katika Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) wametakiwa kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa yanayolenga kuendeleza sekta ya mafuta na gesi asilia, ikiwemo agizo la kuhakikisha mazungumzo ya Mradi wa Kuchakata Gesi kuwa Kimiminika (LNG) yanakamilika kwa wakati ili utekelezaji wake uanze.

Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, amesema hayo tarehe  jijini Mwanza wakati akifunga kikao kazi cha menejimenti ya TPDC kilicholenga kujadili mipango na bajeti ya Shirika kwa mwaka 2026/2027 pamoja na kufanya tathmini ya utendaji kazi wa Shirika.


Aidha,  Salome amelitaka Shirika hilo kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa mafuta ya kutosha, ikiwemo kwa kujenga miundombinu ya hifadhi ya mafuta, kuimarisha shughuli za utafutaji, uzalishaji na usambazaji wa gesi asilia viwandani, kwenye taasisi, majumbani na kwenye magari, pamoja na kukamilisha miradi ya kimkakati ukiwemo wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).
Kuhusu utekelezaji wa Ajenda ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, Mhe. Salome amepongeza jitihada za TPDC katika miradi ya usambazaji wa gesi asilia kama nishati safi ya kupikia katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam, na kulitaka Shirika hilo kuongeza kasi ili kufikia mikoa mingine.

Vilevile ameipongeza TPDC kwa mchango wake katika kuchochea matumizi ya CNG na hivyo kupunguza foleni katika vituo vya kujaza gesi kwenye magari. Amesema juhudi za TPDC pia zimeonekana kupitia ujenzi wa kituo mama cha CNG katika Barabara ya Sam Nujoma, Dar es Salaam, ambacho kinaendelea kuchochea wawekezaji binafsi kuanzisha vituo vyao kutokana na uhakika wa upatikanaji wa gesi. Pia amepongeza utoaji wa idhini kwa kampuni binafsi kuwekeza katika biashara ya CNG.

Katika hatua nyingine, TPDC pia imetakiwa kutokubaki nyuma katika matumizi ya teknolojia na mageuzi ya kidijitali, ikiwemo matumizi ya Akili Mnemba (Artificial Intelligence – AI), mifumo ya kidijitali na uchambuzi wa takwimu kwani Serikali inatarajia TPDC ijipambanue kidijitali ili kurahisisha utoaji wa huduma, kupunguza urasimu, kuongeza uwazi katika manunuzi, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza faida.

No comments