TANZANIA KUWA KITOVU CHA USAFIRISHAJI – WAZIRI MKUU
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema mipango inayoandaliwa na Serikali inalenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, viwanda na biashara katika ukanda wa Afrika.
Amesema Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2026/2027 – 2030/2031 una dhima ya mageuzi kwa ajili ya ukuaji wa uchumi jumuishi na uzalishaji wa ajira na kwamba unatarajiwa kuweka msukumo wa kipekee na kuleta mageuzi yatakayobadilisha mifumo, mitazamo na mwenendo katika utendaji.
“Hatua hii itachochea tija katika uzalishaji, kuongeza uwezo wa nchi katika kushindana kikanda na kimataifa, na kuchochea muunganiko wa sekta mbalimbali. Lengo ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, viwanda na biashara katika ukanda wa Afrika,” amesema.
Ametoa kauli hiyo bungeni leo (Ijumaa, Februari 6, 2026) katika hotuba ya kuhitimisha mkutano wa pili wa Bunge wakati akielezea Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali katika muda wa Kati wa 2026/2027 – 2028/2029 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2026/2027. Bunge limeahirishwa hadi Machi 31, 2026.
Akielezea mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango huo, Waziri Mkuu amesema Serikali itatekeleza vipaumbele katika miradi inayoendelea, iliyosainiwa pamoja na vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
“Maeneo mahsusi ya kipaumbele katika matumizi ni kugharimia miradi ya kielelezo na kimkakati inayoendelea, deni la taifa, mishahara ya watumishi wa umma na huduma za jamii,” amesema.
Akitoa maelekezo katika maandalizi ya Mpango na Bajeti kwa mwaka 2026/2027, Waziri Mkuu amewataka Maafisa Masuuli waweke msukumo kwenye maeneo sita yakiwemo ya kusimamia kusimamia nyongeza ya asilimia tano kwenye mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu inayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Amewataka Maafisa Masuuli wazingatie mkakati wa kulinda wawekezaji wa ndani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika zabuni, masharti ya mikataba na malipo ya hati za madai. Aidha amewataka waandae mikakati ya kuzalisha, kulea na kukuza wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa kupitia dhana ya ushirikishaji wa wananchi katika utekelezaji, uwezeshaji na upatikanaji wa mikopo ya gharama nafuu ili kuwezesha uibuaji wa fursa za ajira kwa vijana.
Pia amezitaka taasisi na mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yaweke mikakati ya kuondokana na utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu ifikapo Juni, 2029 ili kutoa fursa kwa serikali kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo inayowahusu wananchi.
Post a Comment