ULEGA ATANGAZA NEEMA KWA WAHANDISI VIJANA
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza mkakati kabambe wa kukuza ubunifu wa wahandisi wa ndani kwa kuahidi kuzawadia mawazo ya kibunifu yatakayotatua changamoto zilizopo nchini.
Akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Fani za Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Ulega amesema mpango huo utahusu wanafunzi wanaosomea taaluma hizo katika vyuo vikuu vilivyopo nchini.
Amesema mtazamo wa wizara ni kuchochea kada ya wanafunzi wasomi wa uhandisi ambao watakuwa wanajali zaidi kwenye kutatua kero za taifa lao na si kuwa na maandishi mengi yasiyo na mchango kwenye utatuzi wa changamoto.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na Ndani ya Uhandisi na Teknolojia (CoET), Ulega, ametangaza zawadi ya shilingi Milioni-10 itakayogawanywa kwa washindi watatu waliotoa mawazo bora yatakayosaidia jamii.
Amesema Serikali ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan tayari imeahidi kutoa shilingi bilioni 200 kusaidia makundi ya vijana na wanawake na kwamba mpango huu wa wizara yake ni sehemu ya kuongezea kile kilichoanzishwa kwenye uwezeshaji wa makundi hayo.
Naye, Naibu Makamu Mkuu wa UDSM (Taaluma), Profesa Rose Upor, amempongeza Waziri Ulega kwa kukubali kuzungumza na jumuiya ya wanafunzi na kueleza kuhusu mwelekeo wa nchi.




.jpeg)

Post a Comment