ASILIMIA 3 INAYOKATWA UNAPONUNUA UMEME IMELETA MANUFAA-TEF

Miradi ya kusambaza umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini-REA, inaonesha namna makato ya asilimia 3 ya manunuzi ya umeme inavyotumika kuleta maendeleo chanya kwa Watanzania.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania-TEF, Deodatus Balile, wakati wa ziara ya wahariri kutembelea mradi wa kupeleka umeme katika vitongoji 6 vilivyopo ukanda wa Ziwa Nyasa, wilayani Ludewa, mkoani Njombe.

Mradi huo ni ushahidi kuwa michango ya wananchi kupitia makato hayo ya asilimia 3 unaponunua umeme inarejea kwa jamii kwa kugharamia miradi ya maendeleo kupitia REA.

Mradi huo wa kusambaza umeme katika vitongoji 6 unatekelezwa na REA kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1 na ulianza kutekelezwa Julai 13, 2025 huku ukitarajiwa kukamilika Aprili 13, 2026.

Naye, Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Dastan Kalugira, amesema mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni Suma JKT ambaye tayari amekamilisha kazi ya kusimamisha nguzo zote 105 zinazohitajika kwa mradi huo.

Mradi huo utanufaisha wateja wa awali 160, huku Shirika la Umeme Tanzania-TANESCO, likitarajiwa kuendelea kuwaunganisha wateja wengine wapya kwa gharama za REA baada ya kukamilika kwa mradi.

Ingawa mradi huo upo katika Mkoa wa Njombe, lakini baadhi ya vitongoji vinne vilivyopo upande wa ufukwe wa Matema wilayani Kyela mkoani Mbeya, vimeunganishwa umeme kutoka upande huo kutokana na ugumu wa kuvifikia kupitia Ludewa mkoani Njombe.

Vitongoji vitakavyonufaika na mradi huo ni Kitewele na Kimata vilivyopo wilayani Ludewa, pamoja na Kigulu, Chanjale, Lumbira na Nkanda vilivyopo upande wa Matema wilayani Kyela.

Takwimu za Mkoa wa Njombe zinaonesha kuna jumla ya vijiji 381 na vyote vimeunganishwa umeme. Kati ya vitongoji 1,833 vilivyopo mkoani Njombe, vitongoji 1,249 vimepata umeme, huku vitongoji 584 vikiwa bado havijafikiwa na huduma hiyo.

No comments