CHONGOLO ASISITIZA ULINZI WA MRADI WA UMWAGILIAJI MKOMBOZI KWA MANUFAA YA WATANZANIA WOTE

Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesisitiza ulazima wa kulindwa kwa Mradi wa Umwagiliaji Mkombozi uliopo Pawaga mkoani Iringa, akieleza kuwa uwekezaji huo wa serikali unalenga kuongeza uzalishaji wa mpunga, kuinua kipato cha wakulima na kuchangia usalama wa chakula kwa manufaa ya Watanzania wote. 

Chongolo amesema hayo Februari 27 baada ya kutembelea mradi huo wa Umwagiliaji Mkombozi uliopo Pawaga mkoani Iringa na kusisitiza kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuimarisha sekta ya kilimo kupitia matumizi ya teknolojia na miundombinu bora ya Umwagiliaji, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi, hususani wakulima wa eneo hilo, kushiriki kikamilifu katika kuutunza na kuutumia kwa tija ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu. 

Aidha Chongolo amesema serikali haitavumilia biashara ya ardhi ndani ya mradi huo kwa kuwa lengo lake ni kuwainua wakulima kiuchumi kupitia kilimo cha kisasa na chenye tija. 

Naye Mkurugenzi Tume ya Taifa ya Umwagiliaji  (NIRC), Raymond Mndolwa amesisitiza kuwa mifugo haitaruhusiwa kuingizwa ndani ya eneo la mradi kwa kuwa imekuwa chanzo cha uharibifu wa mifereji na kingo zake. 

Akieleza utekelezaji mradi, Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Iringa, Peter Akonaay amesema mradi wa Skimu ya Umwagiliaji Mkombozi unahusisha vijiji sita kati ya vijiji kumi na tano vya Tarafa ya Pawaga na ni uwekezaji mkubwa wa kimkakati.

No comments