HASHEEM THABITI ASHINDA UCHAGUZI NAFASI YA RAIS WA SHIRIKISHO LA MPIRA WA KIKAPU



Uchaguzi wa viongozi wapya wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) umefanyika leo jijini Dodoma, ambapo wajumbe walipiga kura kwa kufuata taratibu za kikatiba za shirikisho hilo na kupata safu mpya ya uongozi itakayoongoza maendeleo ya mpira wa kikapu nchini.


Katika uchaguzi huo, Bw. Hasheem Thabeet Manka alichaguliwa kuwa Rais wa TBF. Akiwa na uzoefu mkubwa katika masuala ya michezo, anatarajiwa kuongoza juhudi za kuimarisha ushindani wa ndani, kukuza vipaji vya vijana na kuimarisha miundombinu ya mpira wa kikapu nchini.


Nafasi ya Makamu wa Rais imechukuliwa na Bw. Mohamed Kasui, ambaye atakuwa msaidizi mkuu wa rais katika kusimamia utekelezaji wa mipango na sera za shirikisho.


Kwa upande wa utendaji, Bw. Mwenze Fiston Kabinda amechaguliwa kuwa Katibu Mkuu, nafasi yenye dhamana ya kusimamia shughuli za kila siku za shirikisho pamoja na uratibu wa mashindano na programu za maendeleo. 


Naye Bw. Simon Mirondo amechaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu.

Uchaguzi huo unatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha uongozi bora na uwajibikaji ndani ya TBF, huku wadau wa mpira wa kikapu wakieleza matumaini yao kuwa uongozi mpya utaongeza kasi ya maendeleo ya mchezo huo, kuimarisha ligi za ndani na kuongeza ushiriki wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa.


Viongozi hao wanatarajiwa kuapishwa na kuanza rasmi majukumu yao mara baada ya kukamilika kwa taratibu zote za kisheria, huku wito ukitolewa kwa wadau wote kushirikiana nao ili kuendeleza mpira wa kikapu nchini.





No comments