KAMATI YA BUNGE TAMISEMI YATAKA FEDHA KUONGEZWA KUKAMILISHA BARABARA ZA PICHANDEGE–SGR NA KONGOWE


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya TAMISEMI imeielekeza Serikali kuongeza fedha ili kukamilisha ujenzi wa barabara za Pichandege–Sofu–Bokomnemela na Kongowe–Forest–Yombo katika Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani, kutokana na umuhimu wake katika kurahisisha usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Florent Kyombo,  ametoa maelekezo hayo baada ya kamati hiyo kukagua miradi hiyo miwili ya barabara iliyo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Machi 14, 2026.

Ameeleza barabara ya Pichandege–Sofu–Bokomnemela itarahisisha wananchi kufika Stesheni ya SGR bila kupitia Dar es Salaam, huku Naibu Waziri wa TAMISEMI, Dkt. Jafar Seif, akisema Serikali imepokea maelekezo hayo na inaendelea kusimamia miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

Mbunge wa Kibaha Mjini, Silvestry Koka, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutenga fedha za barabara, wakati Diwani wa Kata ya Sofu, Mashaka Mahande, akiomba Serikali itoe kipaumbele barabara ya Sofu inayounganisha wananchi na Stesheni ya SGR pamoja na Chuo Kikuu cha TNG. 

Meneja wa TARURA Mkoa wa Pwani, Ibrahim Kibasa, amesema mradi wa barabara ya Sofu–Bokomnemela umefikia asilimia 95 ya utekelezaji tangu uanze Agosti 2024, huku barabara ya Kongowe–Forest–Bagamoyo yenye urefu wa mita 700 nayo ikiwa imefikia asilimia 95 ya utekelezaji.

No comments