MASAUNI: MPANGO WA KUKIJANISHA NCHI UPO MBIONI

Serikali ipo mbioni kuanzisha Mpango wa Mageuzi ya Kijani utakaolenga kukijanisha Tanzania na kuboresha usafi wa mazingira nchi nzima. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Hamad Yussuf Masauni ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza, Machi 13, 2026 ambapo amesisitiza kuwa kila mmoja anaowajibu wa kulinda mazingira na Serikali itawapongeza wale wanaozingatia sheria za Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira na pia kuwachukulia hatua kali wanaoharibu Mazingira.

 

Amesema Mpango huo umegusa takribani maeneo yote ili kuhakikisha Mazingira yanakuwa safi na salama hususani katika upandaji miti ili kuepuka majangwa na kuongeza bustani, usafishaji wa miji, ulinzi wa vyanzo vya maji, utakaochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharibifu wa mazingira na maradhi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda amesema Ofisi yake inafanya juhudi kuhakikisha Mazingira yanalindwa na kutunzwa katika mkoa huo licha ya changamoto zinazoikabili Ofisi hiyo hasa katika udhibiti wa Kelele chafuzi za Maeneo ya kumbi za starehe.

Amesema asilimia 53 ya eneo la Mkoa wa Mwanza linazungukwa na maji hivyo linahitaji uangalizi wa kipekee katika uhifadhi wa mazingira hususan vyanzo vya maji na mwambao wa Ziwa Victoria ili kuhakikisha rasilimali za uvuvi zinaendelea kuwepo.

Katika hatua nyingine Masauni pia alitembelea eneo lililoathirika na mafuriko hivi karibuni na kuharibu miundombinu mbalimbali ikiwemo barabara, nyumba na mali za wananchi.

No comments