KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA TANESCO UTEKELEZAJI WA MRADI WA UMEME JUA KISHAPU
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa Mradi wa Uzalishaji Umeme kwa nguvu ya Jua wa Kishapu wenye uwezo wa Megawati 50 unaotekelezwa katika Mkoa wa Shinyanga.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Subira Mgallu, mara baada ya Kamati kutembelea mradi huo tarehe 13 Machi, 2026 kwa lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji wake pamoja na ufanisi wa matumizi ya fedha zilizotolewa na Serikali.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Mgallu alisema mradi huo ni hatua muhimu katika mageuzi ya sekta ya nishati nchini kutokana na matumizi ya teknolojia ya nishati jadidifu.
Alisema Kamati imeridhishwa na namna fedha zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo zimetumika ipasavyo na kufanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa ufanisi.
Aidha, alisema mradi huo tayari umeanza kuchangia Megawati 50 katika Mfumo wa Gridi ya Taifa, hatua inayochangia kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini pamoja na kuimarisha vyanzo mseto vya nishati.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, alisema mradi wa Kishapu unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza ya Megawati 50 tayari imekamilika na imeanza kuingiza umeme katika Gridi ya Taifa.


.jpeg)


Post a Comment