MADINI YATAMBA NA VIPAUMBELE NANE 2026/2027


WIZARA ya Madini imepanga kutekeleza vipaumbele nane kwa mwaka wa fedha 2026/2027,kuimarisha utafiti wa madini ili kubaini maeneo mapya yenye utajiri na kuongeza takwimu sahihi zitakazowavutia wawekezaji hatua hiyo itaongeza hifadhi ya madini na kuchochea ukuaji wa sekta hiyo.


Akiwasilisha Mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2026-2027, April 27,2026,Bungeni Jijini Dodoma,Waziri wa Wizara hiyo Anthony Mavunde amesema vipaumbele hivyo vinalenga kukuza mchango wa sekta ya madini katika uchumi wa Taifa, kuongeza ajira na kuimarisha usimamizi wa rasilimali.


Vipaumbele vingine ni kukuza uongezaji thamani wa madini kwa kuhakikisha yanachakatwa ndani ya nchi, hatua itakayoongeza mapato, ajira na thamani ya mauzo ya nje.


Kipaumbele cha tatu ni kuendelea kuimarisha ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa madini, ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo na wa kati ili waweze kunufaika zaidi na rasilimali hizo.


Waziri Mavunde amesema pia wataendeleza na kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia maeneo rasmi, mitaji na teknolojia bora, ili kuongeza uzalishaji na kuondoa uchimbaji usio rasmi,kuendelea kuimarisha udhibiti wa mapato yatokanayo na madini kwa kudhibiti utoroshaji na kuhakikisha kodi na tozo zinalipwa kikamilifu.


Wizara hiyo pia itakuza masoko ya madini nchini ili wachimbaji wauze madini yao kwa uwazi na bei yenye ushindani, jambo litakaloongeza mapato ya Serikali na wachimbaji,kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta hiyo kwa kuboresha mazingira ya biashara, ikiwa ni pamoja na kurahisisha utoaji wa leseni na kuweka sera rafiki kwa wawekezaji.


Kipaumbele cha nane ni kuimarisha usimamizi wa mazingira na usalama migodini ili kuhakikisha uchimbaji unafanyika kwa kuzingatia sheria, kulinda afya za wachimbaji na mazingira kwa ujumla.

No comments