MSD YAONGEZA USAMBAZAJI WA DAWA ZA SUMU YA NYOKA
Uwepo wa matukio ya wananchi kung’atwa na Nyoka umeendelea kuwa changamoto katika baadhi ya mikoa, hususan Tabora, Kigoma na Katavi, hali iliyolazimu Bohari ya Dawa-MSD kuongeza juhudi za kusambaza dawa za kukabiliana na sumu ya nyoka katika maeneo hayo.
Licha ya kukosekana kwa takwimu rasmi zinazoonesha ukubwa wa tatizo hilo kwa kila mkoa, mahitaji ya dawa hizo yamekuwa yakiongezeka katika vituo vya afya, ishara ya kuongezeka kwa matukio ya kung’atwa na nyoka katika jamii.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari, Meneja wa MSD Kanda ya Tabora, Rashid Omary, amesema taasisi hiyo imeendelea kuchukua hatua za haraka kuhakikisha upatikanaji wa dawa hizo ili kuokoa maisha ya wananchi.
Katika kipindi cha miezi tisa kuanzia Julai 2025 hadi Machi 2026, MSD Kanda ya Tabora, imesambaza dozi 202 za dawa za kutibu sumu ya nyoka kwa vituo vya afya vilivyowasilisha maombi ya dawa hizo.
Usambazaji huo umefanyika kwa kuzingatia mahitaji halisi kutoka vituo vya afya, hali inayoakisi uwepo wa matukio ya mara kwa mara ya kung’atwa na nyoka katika maeneo husika.
Aidha, MSD itaendelea kuimarisha upatikanaji wa dawa hizo muhimu ili kupunguza madhara na vifo vinavyoweza kusababishwa na sumu ya nyoka.



Post a Comment