MSD YAWAHAKIKISHIA WATANZANIA UHAKIKA WA DAWA LICHA YA MZOZO WA MASHARIKI YA KATI
Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imewahakikishia Watanzania kuwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini uko imara, ukiwa na akiba ya kutosha kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita, licha ya kuendelea kwa mzozo wa Mashariki ya Kati.
Ufafanuzi huo umetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, kufuatia kuibuka kwa wasiwasi miongoni mwa wananchi kuhusu uwezekano wa kupungua kwa dawa na vifaa tiba, hasa kutokana na athari zinazoweza kusababishwa na mvutano wa kijeshi kati ya Marekani na Iran.
Amesema MSD imejipanga vyema kuhakikisha upatikanaji endelevu wa bidhaa hizo muhimu, huku ikieleza kuwa tayari kuna tathmini inayoendelea kufanywa na timu maalumu ya wataalamu ili kubaini hatari zinazoweza kujitokeza na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana nazo.
Aidha, Mkurugenzi huyo amesisitiza kuwa juhudi zinaendelea kuimarishwa, hasa katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi hauathiriki na mabadiliko ya hali ya usalama na uchumi wa kimataifa.
Amesema Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa hali hiyo ili kuhakikisha huduma za afya nchini haziathiriki na kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma bora bila usumbufu.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD alikuwa akizungumza leo katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dodoma akitolea ufafanuzi wa kazi zinazofanywa na taasisi hiyo.



.jpeg)

.jpeg)

Post a Comment