SERIKALI YAELEZA UMUHIMU WA TAASISI ZA ELIMU YA JUU KIUCHUMI
Serikali imesema inatambua jukumu muhimu la taasisi za elimu ya juu katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi kupitia uzalishaji wa rasilimali watu, kuimarisha uwezo wa utafiti, na kukuza ubunifu.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Programu ya Shahada ya Uzamivu (PhD), ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), iliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya KingJada, jijini Dar Es Salaam.
Alieleza kuwa Serikali inatambua wazi utafiti na maendeleo ya sayansi na Teknolojia na Mabadiliko ya Kidijitali kama vigezo muhimu vya mabadiliko ya kitaifa kwa lengo la kuongeza uwekezaji katika utafiti na maendeleo hivyo wataalamu watakaopata ujuzi katika masuala hayo ya kifedha wataisaidia Serikali kuleta maendeleo ya kiuchumi.
‘’Ukiangalia tuna Dira ya mwaka 2050 ambayo tunaiongelea sana ambayo tumeshaanza nayo na ili kutekelezwa maana yake tunahitaji watu wenye uelewa mkubwa wa kwenda nao moja kwa moja kwahiyo tunaamini changamoto ambazo sasa wanafunzi hawa wanaenda kuzitatua kwenye jamii zinaenda pia kusaidia utekeleazji wa Dira yetu ya Maendeleo 2050’’ alisema Mhe. Luswetula (Mb).
Mhe. Luswetula aliziagiza Taasisi za Elimu ya Juu, kuendelea kuwa wabunifu ili kujibu changamoto za kitaifa na kimataifa na kuongeza uwezo wa kutatua changamoto zinazojitokeza katika harakati za kukuza uchumi wa nchi, huku akisisitiza Chuo hicho na vyuo vingine nchini kuendelea kuongeza ubunifu na kuzalisha rasilimali watu wenye ujuzi.
Aliongeza kuwa ni vyema wataalam wa utafiti wakaendelea kufanya utafiti ambao utachangia katika kutatua changamoto halisi katika maeneo mbalimbali ikiwemo, ujumuishaji wa kifedha, uwekezaji na ukuaji wa uchumi, Ufanisi wa sekta ya umma, mabadiliko ya kidijitali na ustahimilivu wa hali ya hewa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha IFM, Profesa Emmanuel Mjema, alieleza kuwa Chuo hicho kimeendelea kujikita katika lengo la kuanzishwa kwake huku akifafanua kuhusu umuhimu wa elimu juu ya masuala ya fedha.
‘’Unajua elimu ya fedha inahitajika katika taasisi zote watu wanafikiria elimu ya fedha wanafikiri labda ni benki na ni Benki Kuu tu lakini kila mahali elimu ya fedha inahitajika. kwahiyo ina maana kwamba wataalamu wa masuala ya fedha mnaowaona wengi asili yake ni IFM’’ alisema Profesa Mjema.
Hafla ya Uzinduzi wa Programu ya Shahada ya Uzamivu (PhD), ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), iliyofanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya KingJada, jijini Dar Es Salaam ilihudhuriwa na wawakilishi kutoka katika ofisi mbalimbali ikiwemo Benki Kuu ya Tanzania (BoT), watumishi wa Chuo hicho, pamoja na wadau mbalimbali wa chuo hicho.








Post a Comment