SILINDE AZINDUA BARAZA LA SITA LA WAFANYAKAZI NIRC
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, amezindua Baraza la Sita la Wafanyakazi la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), huku akitoa wito kwa watumishi wa Tume hiyo kudumisha umoja na kutokubali kukatishwa tamaa na sauti chache za watu wasiothamini kazi nzuri inayofanywa na taasisi hiyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa baraza hilo, Mhe. Silinde amesisitiza kuwa uongozi ni dhamana ya muda na kila mtumishi ana wajibu wa kutimiza sehemu yake kwa uadilifu kabla ya muda wake kukamilika.
Amesema mafanikio yanayoonekana ndani ya Tume hiyo yanatokana na uongozi imara, uwajibikaji wa watumishi pamoja na ushirikiano wa karibu uliopo kazini, jambo lililoongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yake hatua ambayo inaungwa mkono na
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na imai yake ya uwekezaji katika Kilimo cha Umwagiliaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, alibainisha kuwa Tume imejipanga vizuri kwa mwaka wa fedha 2026/2027 katika kukamilisha, kuendeleza na kusimamia miradi iliyopo huku mkazo mkubwa ukiwekwa kwenye uboreshaji wa miradi na ulinzi wa ardhi kwa ajili ya wakulima wadogo.
Bw. Mndolwa amesema kumekuwa na changamoto baadhi ya watu wenye fedha kuanza kuwarubuni wananchi na kuwapora maeneo ya ardhi yenye miradi ya Umwagiliaji baada ya kuona Serikali imeweka miundombinu ya kisasa na maeneo hayo yanaenda kuwa na tija.
Naye Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Mhandisi Saidi Ibrahim, akizungumza katika baraza hilo, amempongeza Mkurugenzi Mkuu na uongozi wake, akimtaja kama mlezi aliyefanikiwa kuimarisha mshikamano kati ya menejimenti na wafanyakazi.
![]() |







Post a Comment