TANZANIA YAFUNGUA MILANGO KWA WAWEKEZAJI
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ally Maulid, ameweka bayana Tanzania imeendelea kuwa kivutio cha uwekezaji kutokana na mazingira rafiki yasiyo na urasimu kwa wawekezaji.
Amesema hayo April 23,2026 wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wakati akiweka jiwe la msingi la kiwanda cha kuunganisha magari cha ROSTAR Tanzania, kwa niaba ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Maulid amesema kufunguliwa kwa milango ya uwekezaji kumeongeza kasi ya ukuaji wa uchumi na ajira nchini, huku Serikali ikiendelea kuboresha miundombinu ya barabara na umeme.
Amebainisha kuwa barabara ya kilometa 1 nukta 7 kuelekea kiwandani hapo itajengwa kwa gharama ya sh.bilioni 3.4, na tayari huduma ya umeme imeimarishwa kupitia njia mbili za msongo wa KV 33 kutoka Mlandizi.
Kwa upande wake,wa taarifa ya Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Bai Xinguo, amesema kiwanda kina uwezo wa kuzalisha magari 5,000 kwa mwaka, na tayari kimepokea oda ya magari elfu moja.
Amesema uwekezaji wa awamu ya kwanza umegharimu dola za Marekani milioni 20, huku mpango ukiwa kuwekeza zaidi ya dola milioni 60 katika hatua zinazofuata.
Ameongeza kuwa kiwanda hicho kimetoa ajira 500, ambapo ajira rasmi ni 300, na kinatarajiwa kupunguza utegemezi wa kuagiza magari kutoka nje ya nchi.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, amesema idadi ya viwanda mkoani Pwani imeongezeka kutoka 1,387 mwaka hadi 1,722 mwaka 2026.
Naye Mwenyekiti wa CCM Bagamoyo, Abubakar Mlawa, ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kuomba bidhaa zinazozalishwa mkoani humo ziwekwe nembo maalum ya kutambulisha zilipotengenezwa.





Post a Comment