SERIKALI YASISITIZA MATUMIZI YA MIFUMO YA KIDIJITALI



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesisitiza matumizi makubwa ya mifumo ya kidijitali katika kuimarisha utendaji kazi serikalini, akielekeza watumishi kuachana na matumizi ya barua za kawaida na badala yake kutumia mifumo ya kielektroniki ikiwemo e-Uhamisho na e-Utendaji.


Akifungua Mkutano wa Pili wa Jumuiya za Wataalamu wa Utawala na Rasilimaliwatu (AAPAM) Tawi la Tanzania, unaofanyika jijini Arusha Mei 5–7, 2026, Waziri Kikwete amesema mageuzi ya utumishi wa umma hayawezi kufikiwa bila matumizi sahihi ya teknolojia yanayozingatia uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.


Amesema mageuzi hayo yanategemea kwa kiasi kikubwa wataalamu wa utawala na rasilimaliwatu, ambao wana jukumu la kuhakikisha taasisi za umma zinakuwa na watumishi wenye uwezo, maadili na uzalendo, huku wakisimamia matumizi bora ya mifumo ya kiteknolojia.


“Mageuzi ya utumishi wa umma siyo tu kubadili mifumo ya kiteknolojia, bali pia kubadili fikra, mitazamo na utamaduni wa utendaji kazi,” amesema.


Katika hotuba yake, amssisitiza umuhimu wa kujenga uwezo wa kidijitali kwa watumishi wa umma, kuvutia na kuendeleza vipaji hasa kwa vijana, pamoja na kuhakikisha mifumo ya teknolojia inaendana na maadili na uwajibikaji.


Akizungumzia kaulimbiu ya mkutano huo inayohusu kufikiria upya utoaji wa huduma za umma kwa kutumia teknolojia, Waziri huyo amesema wataalamu hao wanapaswa kuwa chachu ya mabadiliko katika taasisi zao.


Mkutano huo umewakutanisha wataalamu wa utawala na rasilimaliwatu kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili namna bora ya kuboresha utumishi wa umma barani Afrika.







No comments