MWANAFUNZI AJIFUNGULIA CHOONI NA MTOTO WA MIAKA 6 ALAWITIWA CHALINZE-MORCASE



Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Kibindu ,Chalinze, wilayani Bagamoyo, ,mkoani Pwani amejifungua mtoto wa kike kisha kumtupa kwenye shimo la choo cha mabweni ya wanafunzi wa kike, katika tukio lililoibua taharuki shuleni hapo baada ya mwanafunzi mwenzake kusikia sauti ya mtoto chooni.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema tukio hilo liligundulika Mei 19, 2026 majira ya saa 4:00 asubuhi katika shule hiyo . 


Amesema mwanafunzi huyo alikuwa na ujauzito ambao haukubainika katika kipindi chote cha miezi tisa kutokana na kuvaa majuba hadi alipopatwa na maumivu makali ya tumbo na kwenda chooni, ambako alijifungua mtoto huyo kabla ya kumtupa kwenye shimo la choo.


Morcase ameeleza mwanafunzi mwingine aliingia chooni na kuona matone ya damu karibu na tundu la choo, na alipomwaga maji alisikia sauti ya mtoto ndipo alipotoa taarifa kwa uongozi wa shule.


Ameeleza kuwa kwa kushirikiana na viongozi wa kijiji pamoja na Polisi Kata, jitihada za kumuokoa mtoto zilifanyika na kukimbizwa katika Kituo cha Afya Kibindu kwa matibabu.


Amesema ama na mtoto wanaendelea na matibabu katika Kituo cha Afya Kibindu na baada ya matibabu kukamilika hatua nyingine za kisheria zitafuata. 


Katika tukio jingine, Jeshi la Polisi Mkoani humo linamshikilia Kesi Juma Ibrahim, miaka 22, mkulima na mkazi wa Kifuleta, Chalinze kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa miaka sita (jina linahifadhiwa).


Kwa mujibu wa Morcase tukio hilo lilitokea Mei 17, 2026 majira ya saa 7:00 mchana baada ya mtuhumiwa huyo kumlaghai mtoto ambaye ni jirani yake na kumuingiza chumbani kwake kabla ya kumfanyia kitendo hicho.


Ameeleza wazazi wa mtoto walipogundua tukio hilo walitoa taarifa Kituo cha Polisi Mbwewe ambapo mtuhumiwa alikamatwa na upelelezi unaendelea kabla ya kufikishwa mahakamani.

No comments