TANZANIA NA JAPAN KUFUNGUA MILANGO MIPYA YA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA NISHATI
Ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika sekta ya nishati unaingia hatua mpya, huku juhudi zikielekezwa zaidi katika kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi na teknolojia za kisasa za uzalishaji umeme.
Hatua hiyo imebainishwa jijini Dar es Salaam Aprili 30,2026 wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia,Dkt. James Mataragio alipokutana na Mwakilishi Mkuu mpya wa Japan International Cooperation Agency, Dkt. Kuge Katsuya ambapo ameweka wazi Mkakati wa Serikali kuifanya sekta ya nishati kuwa kivutio kikubwa cha mitaji ya kimataifa hususan kutoka Japan.
Akizungumzia ushirikiano wa Tanzania na Japan Dkt. Mataragio amesema JICA imekuwa mdau wa muda mrefu katika sekta ya nishati nchini na wameshiriki katika miradi ya Uandaaji wa Mpango kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia Nchini wametoa fursa za kuwajengea uwezo wataalamu katika Matumizi ya gesi asili pamoja na utekelezaji wa Miradi mbalimbali ya umeme.
Aidha Dkt. Mataragio amekumbushia ahadi ya muda mrefu ya Japan ya kuwezesha Mradi wa umeme wa megawati 300 mkoani Mtwara.
Kwa upande wake, Dkt. Kuge ameashiria mwelekeo mpya wa ushirikiano utakaojikita katika Mafunzo ya teknolojia ya nishati ya nyuklia, Uzalishaji wa umeme kupitia gesi asilia kwa ufanisi mkubwa zaidi na Kuunganisha Tanzania na wawekezaji binafsi kutoka Japan
Ahadi hiyo inaashiria uwezekano wa Tanzania kunufaika na teknolojia za kisasa zaidi za nishati kutoka Japan, moja ya nchi zinazoongoza duniani katika ubunifu wa nishati.
Mkutano huo umeonesha wazi kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Japan hauishii katika misaada, bali sasa unaelekea kwenye uwekezaji mkubwa na ubadilishanaji wa teknolojia hatua inayoweza kubadilisha kabisa sekta ya nishati nchini





Post a Comment