KIWANDA KIKUBWA CHA KUZALISHA BIDHAA ZA CHUMA KUJENGWA NALA, JIJINI DODOMA
Uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha kisasa cha kuzalisha bidhaa za chuma unatarajiwa kuanza katika eneo la Nala, jijini Dodoma, hatua inayotajwa kuchochewa na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyoendelea kuimarishwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza Juni 15, 2026 jijini Dodoma baada ya mazungumzo na wawekezaji wa Kampuni ya A1 Iron & Steel Tanzania Ltd, Waziri wa Madini Anthony Mavunde alisema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuhimiza uongezaji thamani wa madini nchini ili kupunguza utegemezi wa usafirishaji wa madini ghafi kwenda nje.
Alisema kiwanda hicho, kitakachogharimu takribani shilingi bilioni 600, kinatarajiwa kutumia chuma ghafi kama malighafi kuu katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo mabati, waya wa kufungia nondo, wavu wa nondo na misumari.
Mavunde alieleza kuwa uwekezaji huo unaendana na azma ya taifa ya kujitosheleza katika uzalishaji wa chuma na bidhaa zake, huku ukitarajiwa kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi na kupunguza gharama za bidhaa hizo kwa watumiaji wa ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa A1 Iron & Steel Tanzania Ltd, Himanshu Tiwari, alisema kiwanda hicho kitakuwa cha mfano kwa kutumia teknolojia ya Blast Furnace inayowezesha uzalishaji kuanzia hatua ya malighafi hadi bidhaa za mwisho. Aliongeza kuwa ujenzi wake unatarajiwa kuanza Julai 2026 na kukamilika ndani ya miezi 15, huku ukizalisha ajira takribani 1,500 na kusaidia kuongeza uzalishaji wa bidhaa za chuma kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.






Post a Comment