TEEMO YAZINDUA KITUO CHA UKUSANYAJI WA PLASTIKI KUKABILI TISHIO LA UCHAFUZI WA BAHARI MAFIA



Uchafuzi wa mazingira unaotokana na taka za plastiki zinazotupwa ovyo baharini umeendelea kuwa tishio kubwa kwa mifumo ya ikolojia ya bahari, viumbe wa majini na shughuli za kiuchumi zinazotegemea rasilimali hizo, ikiwemo uvuvi, utalii na kilimo cha mwani katika fukwe mbalimbali ikiwemo Mafia.


Kutokana na changamoto hiyo, Shirika la Harakati na Uwezeshaji wa Mazingira Tanzania (TEEMO) limezindua rasmi Kituo cha Ukusanyaji na Urejelezaji wa Plastiki katika eneo la Kibaoni, Kata ya Kiegeani, wilayani Mafia kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa taka za plastiki, kupunguza uchafuzi wa mazingira ya bahari na kukuza uchumi wa mzunguko (circular economy) katika jamii za visiwani.


Mradi huo unafadhiliwa na kampuni ya C-Weed Mwani kwa kushirikiana na Cargill, wadau wanaoshiriki katika juhudi za kulinda mazingira, kusaidia jamii za pwani na kuendeleza uchumi wa buluu. 


Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Wilaya ya Mafia ambaye pia ni Ofisa Afya wa Wilaya, Othman Masanga, amewaomba wadau wengine kuendelea kuibua miradi endelevu itakayosaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuifanya Mafia kuwa mfano wa utunzaji wa mazingira ya bahari.


Mkurugenzi Mtendaji wa TEEMO, Winfrida Shonde, amesema kituo hicho ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa shirika hilo wa kupambana na uchafuzi wa plastiki na kulinda mazingira ya pwani kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Nae Kombo Mzee, kijana kutoka Kata ya Kilindoni, amefafanua mradi huo ni fursa muhimu kwa vijana kushiriki katika utunzaji wa mazingira huku wakijifunza mbinu za urejelezaji wa plastiki.







No comments