DIPLOMASIA YA UTAMADUNI YACHANUA BUSAN: TANZANIA NA JAPAN ZAPANGA KUIMARISHA USHIRIKIANO KATIKA URITHI WA DUNIA



Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika UNESCO, Mhe. Saidi Yakubu, amekutana na Waziri wa Nchi wa Japan anayeshughulikia Mambo ya Nje, Mhe. Iwao Horii, pembezoni mwa Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO kinachoendelea jijini Busan, Jamhuri ya Korea, tarehe 22 Julai 2026.


Katika mazungumzo hayo, Waziri Horii aliambatana na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Japan katika UNESCO, Mhe. Takehiro Kano. Viongozi hao walijadiliana kuhusu njia za kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Japan katika uhifadhi wa Urithi wa Dunia, maendeleo ya utamaduni na utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu kupitia UNESCO.


Balozi Yakubu aliishukuru Serikali ya Japan kwa mchango wake mkubwa katika kuhifadhi urithi wa utamaduni nchini Tanzania, hususan kupitia ufadhili wa ukarabati wa Jumba la Sinema la Majestic, Zanzibar. Aidha, aliipongeza Japan kwa kuendelea kuunga mkono miradi ya uhifadhi wa maeneo ya Urithi wa Dunia barani Afrika, hatua ambayo imekuwa na mchango muhimu katika kulinda historia, utamaduni na urithi kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.


Mazungumzo hayo pia yalijikita katika fursa za kupanua ushirikiano kupitia programu za kujengea uwezo wataalamu wa urithi, kubadilishana uzoefu wa kitaalamu, pamoja na kuanzisha na kuendeleza miradi ya pamoja ya uhifadhi na usimamizi endelevu wa maeneo ya Urithi wa Dunia nchini Tanzania.


Vilevile, Balozi Yakubu alimkaribisha Mhe. Horii kutembelea Tanzania ili kujionea maeneo mbalimbali ya Urithi wa Dunia yaliyosajiliwa na UNESCO, pamoja na fursa zilizopo katika sekta za utamaduni, urithi na utalii wa kiutamaduni.

Katika kikao hicho, Balozi Yakubu aliambatana na Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Taifa ya UNESCO Tanzania, Profesa Hamisi Malebo, pamoja na maafisa wengine waandamizi wa ujumbe wa Serikali ya Tanzania unaoshiriki Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia.


Kikao hicho kinaendelea hadi tarehe 29 Julai 2026, kikijadili masuala mbalimbali yanayohusu ulinzi, uhifadhi na usimamizi endelevu wa maeneo ya Urithi wa Dunia

No comments