DKT. KIJAJI AAGIZA TATHMINI YA MAENEO YA UHIFADHI KUPUNGUZA MIGONGANO YA BINADAMU NA WANYAMAPORI



Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, ameagiza Bodi ya Menejimenti ya Taasisi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) kufanya tathmini ya kina ya maeneo ya uhifadhi na kuimarisha usimamizi wake ili kupunguza migongano kati ya wananchi na wanyamapori wakali na waharibifu.

Akizungumza Julai 7, 2026 mkoani Morogoro alipokutana na Bodi ya Menejimenti ya TAWA, Dkt. Kijaji amesema ni muhimu kuhakikisha shughuli za kibinadamu kama kilimo, ufugaji na ujenzi wa makazi hazifanyiki karibu au ndani ya maeneo ya hifadhi, hatua itakayosaidia kulinda maisha ya wananchi pamoja na kuhifadhi rasilimali za wanyamapori.

Katika kukabiliana na ujangili, Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa kuandaa mikakati madhubuti ya utoaji elimu kwa umma na kuwashirikisha wananchi katika shughuli za uhifadhi ili wajione kuwa sehemu ya kulinda rasilimali hizo na kuchangia kupunguza vitendo vya ujangili.

Aidha, amesema Serikali inalenga kutekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za taifa ifikapo mwaka 2030 kupitia usimamizi endelevu wa maeneo ya hifadhi.

Dkt. Kijaji pia ameitaka TAWA kuweka mikakati ya muda mfupi, wa kati na wa muda mrefu katika kukabiliana na migongano ya binadamu na wanyamapori, sambamba na kuweka malengo yanayopimika katika vita dhidi ya ujangili na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato kupitia usimamizi bora wa rasilimali za wanyamapori.

Vilevile, amewataka askari wa uhifadhi kujenga mahusiano mazuri na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi kwa kutoa huduma kwa weledi na ushirikiano, huku akiipongeza TAWA kwa mafanikio yaliyopatikana katika maeneo ya uwekezaji na kuitaka kuendelea kusimamia kwa ufanisi maeneo yote ya uwekezaji pamoja na WMAs.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, amesema Bodi ya TAWA imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, huku Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mej. Jenerali Semfuko, akiahidi kuendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali ili kuimarisha usimamizi wa rasilimali za wanyamapori nchini.

















No comments