BOT YAHIFADHI DHAHABU YENYE THAMANI YA SH. TRILIONI 9.76 KATIKA MIEZI 18
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imefanikiwa kununua na kuhifadhi takriban tani 28 za dhahabu zenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.68, sawa na shilingi trilioni 9.76, ndani ya kipindi cha miezi 18, hatua inayolenga kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, kulinda thamani ya shilingi na kuongeza uthabiti wa sekta ya fedha nchini.
Akizungumza katika mjadala kuhusu Mikakati ya Ununuzi wa Dhahabu wa Benki Kuu uliofanyika katika Mkutano wa African Caucus 2026 mjini Banjul, Gambia, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, alisema mpango huo umeiwezesha Tanzania kujenga akiba ya dhahabu kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha uchumi na kuongeza uwezo wa taifa kukabiliana na misukosuko ya kifedha duniani.
Alisema utekelezaji wa mpango huo umeleta mafanikio makubwa katika sekta ya madini kwa kuongeza urasimishaji wa biashara ya dhahabu na kuwawezesha wachimbaji wadogo pamoja na wafanyabiashara kushiriki zaidi katika mfumo rasmi wa kifedha. Kupitia mpango huo, zaidi ya akaunti 4,000 zimefunguliwa katika taasisi mbalimbali za fedha, hatua iliyoongeza ujumuishi wa kifedha nchini.
Gavana Tutuba alibainisha kuwa Benki Kuu imeendelea kuvutia wachimbaji na wafanyabiashara kuiuzia dhahabu kutokana na kutoa bei inayolingana na soko la kimataifa la London na kufanya malipo ndani ya saa 24 baada ya kukamilika kwa mauzo.
Mjadala huo ulikuwa sehemu ya Mkutano wa African Caucus 2026 unaozikutanisha nchi 54 za Afrika kujadili masuala ya uchumi, fedha na maendeleo kwa ushirikiano na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ukiwashirikisha viongozi mbalimbali wa sekta ya fedha na uchumi wanaowakilisha Tanzania katika majadiliano ya kimataifa kuhusu mageuzi ya uchumi na maendeleo ya Bara la Afrika.








Post a Comment