RAIS DKT. MWINYI AKUTANA NA BALOZI WA PALESTINA, AWAKARIBISHA WAWEKEZAJI KUWEKEZA ZANZIBAR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo tarehe 01 Julai 2026, amekutana na Balozi wa Palestina nchini Tanzania, Mhe. Salam Abu Sharar, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo maalum yaliyolenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Zanzibar na Palestina.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Mwinyi amewakaribisha wawekezaji kutoka Palestina kuja kuwekeza Zanzibar katika sekta mbalimbali zenye fursa, ikiwemo nishati, mafuta na gesi, utalii pamoja na Uchumi wa Buluu.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na kuimarisha ushirikiano na washirika wa maendeleo katika utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa wananchi na ukuaji wa uchumi wa Zanzibar.
Kwa upande wake, Balozi wa Palestina nchini Tanzania, Mhe. Salam Abu Sharar, amesema Palestina ina dhamira ya kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi na Zanzibar, kwa kutambua nafasi yake muhimu katika maendeleo ya kikanda.
Aidha, amesema Palestina itaendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria uliopo kati ya pande hizo mbili, sambamba na kubaini maeneo mapya ya ushirikiano yatakayowanufaisha wananchi wa Zanzibar na Palestina.

Post a Comment