RAIS DKT. SAMIA ATOA VIPAUMBELE KWA KATIBU MKUU MPYA AFYA, ASISITIZA DAWA, BAJETI NA UTOAJI WA HUDUMA BORA

 


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemtaka Katibu Mkuu mpya wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, kuhakikisha sekta ya afya inafikia malengo yaliyowekwa kwa kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa bajeti, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.


Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya kumuapisha Dkt. Magembe leo Julai 1, 2026, Rais Samia amesema wizara hiyo ina jukumu kubwa la kuhakikisha fedha zilizoidhinishwa na Bunge zinaleta matokeo yanayoonekana katika kuboresha huduma za afya nchini.


Rais amesema wananchi wanatarajia kuona dawa na vifaa tiba vinapatikana katika hospitali, vituo vya afya na zahanati, hivyo uongozi wa wizara unapaswa kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mipango hiyo ili uwekezaji unaofanywa na Serikali utoe manufaa yaliyokusudiwa.


Aidha, amesisitiza umuhimu wa kujenga mazingira mazuri ya kazi kwa watumishi wa wizara kwa kushirikiana nao, kuwasikiliza na kuwaongoza kwa haki, akieleza kuwa mafanikio ya sekta ya afya yanategemea ushirikiano wa timu nzima.


Rais Samia pia amemhakikishia Dkt. Magembe ushirikiano kutoka Serikalini katika kutekeleza majukumu yake, akisema lengo kuu ni kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuboreshwa na kuwafikia Watanzania kwa ubora na kwa wakati.


Dkt. Grace Magembe anaanza majukumu hayo akiwa na uzoefu mkubwa katika sekta ya afya baada ya kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi, zikiwemo Mganga Mkuu wa Serikali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI.











No comments