RAIS DKT. MWINYI KUONGOZA HAFLA YA KUWASILISHA TAMKO LA PAMOJA LA MARIDHIANO YA KISIASA ZANZIBAR
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuongoza hafla ya kuwasilisha Tamko la Pamoja la Maridhiano ya Kisiasa Zanzibar itakayofanyika Julai 9, 2026, saa 4:00 asubuhi katika viwanja vya Ikulu, Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu Zanzibar, hafla hiyo inalenga kuwasilisha rasmi tamko la makubaliano ya maridhiano ya kisiasa baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo. Hatua hiyo inalenga kuimarisha maridhiano, mshikamano, utulivu wa kisiasa, amani na ustawi wa Zanzibar.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi pamoja na Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud Othman, watasaini Tamko la Pamoja na kushuhudia utiaji saini wa ajenda zilizokubaliwa na pande zote mbili kwa ajili ya utekelezaji wake.
Hafla hiyo itahudhuriwa na viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, viongozi wa vyama vya siasa, wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, wawakilishi wa taasisi za kiraia pamoja na waandishi wa habari.
Aidha, hafla hiyo itarushwa mubashara kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii kwa mujibu wa utaratibu uliopangwa.


Post a Comment