TANZANIA NA MAURITIUS KUIMARISHA USHIRIKIANO WA BIASHARA, UWEKEZAJI NA UCHUMI WA BULUU
Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Mauritius yanatarajiwa kuimarika zaidi kufuatia hatua ya Balozi wa Tanzania nchini Mauritius, Kamishna wa Polisi (CP) Suzan Kaganda, kukutana na Rais wa Jamhuri ya Mauritius, Dharambeer Gokhool, baada ya kuwasilisha Hati zake za Utambulisho katika hafla iliyofanyika Julai 6, 2026, Ikulu ya Serikali, Reduit.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili, hususan katika sekta za biashara, uwekezaji, utalii na Uchumi wa Buluu. Rais Gokhool alimpongeza Balozi Kaganda kwa uteuzi wake na kumhakikishia ushirikiano wa Serikali ya Mauritius katika kutekeleza majukumu yake ya kidiplomasia.
Kwa upande wake, Balozi Kaganda alieleza dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano wa maendeleo kati ya mataifa hayo mawili kwa manufaa ya wananchi wake. Aidha, Balozi Kaganda, ambaye makazi yake ya kikazi yako Harare nchini Zimbabwe, anaendelea kuiwakilisha Tanzania nchini Zimbabwe pamoja na Mauritius.










Post a Comment