TANZANIA YAWEKA MSISITIZO WA TEKNOLOJIA NA UBUNIFU KAMA NGUZO YA UCHUMI WA BAADAYE
Serikali imeeleza kuwa matumizi ya teknolojia za kisasa, akili unde (Artificial Intelligence), utafiti na ubunifu ni miongoni mwa maeneo yatakayobeba ukuaji wa uchumi wa Tanzania katika miaka ijayo, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Akizungumza katika hafla ya utoaji wa Tuzo za Jubilei ya Dhahabu ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, alisema ni wakati wa kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya viwanda na biashara kwa kuwekeza katika uzalishaji wa bidhaa zenye thamani kubwa na kutumia teknolojia za kisasa ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania.
Alisisitiza kuwa utafiti, ubunifu, matumizi ya akili unde, biashara za kidijitali na mifumo ya kisasa ya uzalishaji vinapaswa kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa kukuza uchumi na kuongeza nafasi ya Tanzania katika soko la kimataifa.
Makamu wa Rais pia alitoa wito kwa wazalishaji nchini kutumia alama ya Made in Tanzania ili kujenga utambulisho wa bidhaa za Tanzania na kuongeza uwezo wake wa kushindana katika masoko ya Afrika na duniani.
Aidha, alizitaka taasisi za fedha kuongeza uwekezaji katika sekta ya viwanda, hususan kwa kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa viwanda vidogo na vya kati, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili wajasiriamali wengi katika kupata mitaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, alisema mafanikio ya Maonesho ya Sabasaba kwa kipindi cha miaka 50 yametokana na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi, huku akiwapongeza wafanyabiashara, wazalishaji, wawekezaji na wadau mbalimbali waliochangia mafanikio hayo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Dkt. Latifa Khamis, alisema maonesho hayo yamezalisha fursa za biashara zenye thamani ya shilingi trilioni 129.2 katika kipindi cha miaka 50, hatua iliyochangia kukuza uchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika biashara ya kimataifa.














Post a Comment