WAZIRI HOMERA APIGA MARUFUKU TOZO ZINAZODAIWA KUTOZWA AKINA MAMA WANAOJIFUNGUA SUMBAWANGA



Waziri wa Katiba na Sheria, Juma Zuberi Homera, amepiga marufuku utaratibu unaodaiwa kuwatoza akina mama fedha wanapojifungua katika Hospitali ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, akisisitiza kuwa huduma za afya zinapaswa kutolewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo ya Serikali.

Waziri Homera alitoa kauli hiyo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mtowisa, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, baada ya wananchi kulalamikia kuwa akina mama wanaojifungua watoto wa kiume hutozwa shilingi 10,000 huku wanaojifungua watoto wa kike wakitozwa shilingi 5,000.

Amesema hakuna mtumishi wa umma anayepaswa kuweka au kutoza fedha ambazo hazijaidhinishwa, na kuwataka watumishi wote wa sekta ya afya kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria za utumishi wa umma.

Aidha, Waziri Homera amezielekeza mamlaka zinazohusika kufanya uchunguzi wa haraka kuhusu madai hayo na kuchukua hatua stahiki dhidi ya watakaobainika kukiuka taratibu, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa haki, usawa na bila kutozwa tozo zisizo halali.






No comments