SERIKALI YAWEKA MALIPO YA KIDIJITALI KUZUIA UTAKATISHAJI WA FEDHA.
Serikali imeweka utaratibu wa kutumia njia za malipo ya kidijitali katika miamala mbalimbali nchini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupunguza matumizi ya fedha taslimu na kuziba mianya ya utakatishaji wa fedha haramu.
Hatua hiyo imewekwa kupitia marekebisho ya Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Sura ya 442, pamoja na amri inayobainisha miamala inayopaswa kufanyika kwa njia za kielektroniki.
Akizungumza wakati wa mafunzo kwa Mawakili wa Serikali kuhusu mabadiliko yaliyotokana na Sheria ya Fedha ya mwaka 2026, Mkurugenzi Msaidizi wa Divisheni ya Uandishi wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD), Chresencia Mathayo, amesema hatua hiyo inalenga kujenga mfumo wa malipo ulio salama na unaoweza kufuatiliwa kwa urahisi, hivyo kusaidia kudhibiti utakatishaji wa fedha haramu, ukwepaji wa kodi na uhalifu mwingine wa kifedha.
Amesema amri hiyo inatambua njia mbalimbali za malipo ya kidijitali ikiwemo fedha kwa simu, uhamisho wa fedha kupitia benki, kadi za malipo, mashine za POS, huduma za benki kwa njia ya mtandao au simu pamoja na mifumo ya malipo ya Serikali na kwamba miamala inayopaswa kufanyika kidijitali ni pamoja na malipo ya ada za shule, nauli za usafiri, huduma za maduka makubwa, hoteli, migahawa, utalii,ununuzi na uuzaji wa majengo, mashamba, viwanja, magari na mazao ya kimkakati kupitia AMCOS.
Aidha, amesema Kanuni za Utoaji wa Leseni za Biashara zimerekebishwa ili waombaji wa leseni mpya na wanaohuisha leseni zao waambatishe uthibitisho wa matumizi ya mfumo wa malipo ya kidijitali, ikiwemo Lipa Namba au TANQR na kwamba wafanyabiashara wasiokuwa na mfumo huo hawataweza kuhuisha leseni zao hadi watakapokuwa wamekidhi sharti hilo.
Chresencia amesema maboresho hayo pia yanalenga kupunguza gharama na hatari zinazotokana na matumizi ya fedha taslimu, ikiwemo gharama za kutunza na kusafirisha fedha pamoja na hatari ya wizi na upotevu wa fedha na kwamba mabadiliko hayo yameanza kutumika rasmi Julai 1, 2026,hivyo kuwataka wananchi, wafanyabiashara pamoja na watoa huduma kutumia njia rasmi za malipo ya kidijitali katika miamala iliyobainishwa
.jpeg)
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


Post a Comment