BANDARI YA DAR ES SALAAM YAONGEZA UWEZO WA KUHUDUMIA SHEHENA, YALENGA TANI MILIONI 62

 


Bandari ya Dar es Salaam imeongeza kiwango cha shehena inayohudumiwa kutoka tani milioni 23.7 katika mwaka wa fedha 2023/24 hadi tani milioni 33.7 mwaka 2025/26, huku ikilenga kuongeza uwezo huo hadi tani milioni 62 ifikapo mwaka 2031.


Akizungumza jijini Dar es Salaam na Jukwaa la Wahariri Tanzania-TEF, Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus, amesema ongezeko hilo limetokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuboresha miundombinu ya bandari, ikiwemo kuongeza kina cha bandari, kuboresha magati na kuimarisha miundombinu mingine muhimu.


Amesema matumizi ya vifaa vya kisasa pia yameongeza ufanisi katika upokeaji na uondoshaji wa shehena, hali iliyosaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa muda ambao meli za makasha zinatumia kusubiri na kuhudumiwa bandarini, ambapo muda wa meli hizo umepungua kutoka zaidi ya siku 30 hadi wastani wa siku tatu.


Aidha, amesema ujenzi wa matenki ya kupokea na kuhifadhi mafuta wenye thamani ya shilingi bilioni 678 unatarajiwa kuongeza ufanisi zaidi kwa kupunguza muda wa meli za mafuta kukaa bandarini, pamoja na kupunguza gharama zinazowakabili wafanyabiashara na watumiaji.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania-TEF, Deodatus Balile, amesema ziara ya wanahabari katika Bandari ya Dar es Salaam imewapa fursa ya kujionea hali halisi ya uendeshaji wa shughuli za bandari.


Balile amesema ziara hiyo imekuja pia kufuatia taarifa zilizokuwa zikisambaa kuhusu madai ya kuwepo kwa mizigo iliyokwama na kutotoka bandarini, hivyo wanahabari wamepata fursa ya kujionea hali halisi na kupata ufafanuzi kutoka kwa uongozi wa bandari.






No comments