NEMC YATOA WITO UTUNZAJI WA MAZINGIRA KUELEKEA MVUA ZA EL NIÑO



Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka Watanzania kuchukua tahadhari na kuimarisha utunzaji wa mazingira kuelekea kipindi cha mvua za El Niño, kufuatia tahadhari iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kaimu Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa NEMC, Bi. Martha Kawishe, amesema wananchi wanapaswa kulinda mazingira katika kipindi hiki ambacho mvua zinatarajiwa.


Amesema utupaji holela wa taka, kuziba kwa mifereji, ujenzi katika njia za asili za maji na uharibifu wa maeneo oevu vinaweza kuongeza hatari ya mafuriko. Amesema maeneo ya mabondeni, kingo za mito, maeneo yenye miteremko pamoja na maeneo yenye mifumo duni ya kupitisha maji yanahitaji tahadhari zaidi, huku wananchi wakitakiwa kutotupa taka kwenye mifereji, mito na makorongo.


NEMC pia imezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha njia za maji zinasafishwa na kubaki wazi, huku ikisisitiza umuhimu wa kulinda kingo za mito, mabonde na maeneo oevu pamoja na kuchukua hatua za kuzuia mmomonyoko wa udongo. Hatua hizo zinatajwa kuwa muhimu katika kupunguza athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua kubwa.


Aidha, Baraza limewataka waendelezaji wa miradi, viwanda, vituo vya mafuta, migodi, hospitali na maeneo yanayohifadhi kemikali au taka hatarishi kuhakikisha shughuli hizo zinasimamiwa kwa usalama. Lengo ni kuzuia kemikali na taka hatarishi kusombwa na maji ya mafuriko na kusababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji au kuhatarisha makazi ya wananchi.


Baraza limesema litaendelea kushirikiana na Serikali za Mitaa na taasisi nyingine katika kutoa elimu, kufanya ufuatiliaji na ukaguzi wa mazingira, pamoja na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria dhidi ya shughuli zinazoharibu mazingira. NEMC imewahimiza Watanzania kufuatilia taarifa rasmi za TMA na kuchukua hatua mapema, ikisisitiza kuwa kulinda mazingira ni hatua muhimu katika kupunguza athari za mvua kubwa na mafuriko.





No comments