NAIBU WAZIRI MAHUNDI AWAHIMIZA WANAWAKE MAGEREZA KUJENGA UWEZO, KUTUMIA FURSA ZA KIDIJITALI
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka wanawake wa Jeshi la Magereza kuendelea kujijengea uwezo kwa kuongeza elimu na ujuzi, ili kupata nafasi mbalimbali za uongozi na kitaaluma katika Jeshi hilo.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa wanawake hao kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kutumia fursa za kidijitali katika utekelezaji wa majukumu yao.
Mahundi ametoa kauli hiyo Septemba 7, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza Tanzania 2026, unaolenga kuwajengea uwezo wanawake, kukuza uongozi, kuimarisha usawa wa kijinsia na kuongeza ufanisi katika majukumu ya urekebishaji wa wafungwa.
Amesema uwezeshaji wa wanawake ni sehemu muhimu ya kujenga mtaji watu wenye uwezo, huku akiwataka wanawake wa Jeshi la Magereza kuwa mstari wa mbele katika mageuzi ya kijamii na kidijitali ya Jeshi hilo.
Kwa upande wake, Kamishna wa Divisheni ya Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP Nicodemus Menyiansumba Tenga, amesema mafanikio ya wanawake waliopo katika nafasi mbalimbali ndani ya Jeshi hilo ni mfano unaopaswa kuhamasisha wengine.
Akisoma taarifa ya Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza Tanzania (TPSWNet), Kamishna wa Huduma za Urekebishaji Jeshi la Magereza, CP Amina Jumanne Kavirondo, amesema mtandao huo umeendelea kuwa chombo muhimu katika kuwajengea wanawake uwezo, kukuza usawa wa kijinsia katika majukumu ya kazi, kuweka mazingira rafiki ya kazi kwa wanawake na kuhakikisha uwakilishi wao ndani na nje ya Jeshi pale inapowezekana.

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


Post a Comment